Unyanyapaa Kikwazo Kikuu kwa Waraibu Wa Pombe na Dawa za Kulevya Kutafuta Msaada na Matibabu
Na Rebecca Barasa
Japo kuwa matumizi ya pombe na dawa za kulevya ni hali sugu ambazo zinaweza tibika, tafiti zinaonyesha kuwa waathiriwa wanakabiliana na ubaguzi pamoja na unyanyapaa (seti ya mitazamo hasi na fikra potovu) ambao unaweza kuathiri afya na ustawi wao kwa njia nyingi.
Kuna njia salama, na bora za kuokoa maisha ya waraibu ambazo zinaweza kutumika bila kuumiza hisia za watu wanaojitokeza na kuelezea hali zao za uraibu, changamoto wanazopitia na kufikia azma ya kuomba msaada na kuchagua matibabu kama njia mwafaka. Hata hivyo, unyanyapaa mara nyingi huchangia kama sababu kuu ya waathiriwa kuapa kutotafuta matubabu na hata kupelekea kuwepo na visa vingi vya msongo wa mawazo.
Watu wanaogopa kufichua hali zao za matumizi ya mihadarati kwa kuhofia unyanyapaa watakaokumbana nao kutoka kwa wale wanaowazunguka. Ikiwa mtu ataficha hali kama hii katika mazingira ya matibabu, nayo sababu ikiwa ni kuogopa kudhaliliswa au kuhudumiwa vibaya, anaweza kukosa fursa muhimu za utunzaji na matibabu faafu. Kwa mfano, matabibu huenda wasijue kutoa maelezo kuhusu jinsi mihadarati inavyoweza kuingiliana na kuathiri kufanya kazi kwa dawa walizoandikiwa au huenda wasiichunguzwe ili kubaini hali za kiafya zinazohusiana na matumizi ya dawa za kulevya, kama vile HIV/AiDs, Hepatitis na ugonjwa wa akili. Wanawake wajawazito hasa wanaweza kuepuka kuzungumza kuhusu hali yao ya matumizi ya dawa za kulevya, kuhisi aibu na kuogopa kutokubaliwa na jamii au kupoteza haki za mzazi.
Yapo mambo mengi ambayo wanapitia katika jamii na familia kwa ujumla ambayo yanawafanya waathiriwa kuhisi kana kwamba wamepuuzwa,kubaguliwa, kutengwa na hamna wa kuwajali na kuwaonyesha upendo.kutengwa na familia pamoja na jamii ni hatua ambayo inawapa msukumo na motisha ya kuonelea kuwa, ni heri kuendelea na familia ya waraibu wenzao ambao wanawaenzi kuliko kuteseka katika jamii ambayo haina ukubalifu .Watu walio na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya wanaweza kuhisi kama walio na hatia na kuanza kujilaumu kwa ugonjwa wao. Wanaweza kuwa na unyanyapaa wa kibinafsi, au kuwa na mitazamo hasi kuhusu matumizi yao ya dawa za kulevya. Hisia hizi za aibu na kutengwa zinaweza kuimarisha utaftaji wa dawa za kulevya na kuzama katika lindi hili. Mambo kama haya huwafanya kupoteza mwelekeo katika maisha na hata kujitia kitanzi.
Maneno yanayotumiwa kuwarejelea walio na uraibu mara nyingi huonyesha dhana potofu kwamba matumizi yao ya dawa na tabia zinazohusiana na ulevi ni chaguo la mtu binafsi, sio hali ya kulazimishwa, na kwamba wao ndio wa kulaumiwa kwa hali yao ya kiafya. Uchunguzi unaonyesha kuwa maneno kama vile "junky, addict, pothead na zombie" huchochea upendeleo hasi na kuwadhoofisha watu.Lugha inaweza kushawishi mitazamo ya matabibu. Katika utafiti mmoja, matabibu walimkadiria mtu aliyeelezewa kuwa"mtumia dawa vibaya” kama anayestahili kulaumiwa na kuadhibiwa kuliko mtu anayeelezewa kuwa "mwenye ugonjwa wa matumizi ya dawa."
Kila mtu anapaswa kuwa kwenye msitari wa mbele, kushtumu vikali jambo la kuwapachika majina wanaotumia mihadarati. Unapowasikia watu wakitoa maoni mabaya au yasiyo sahihi, unapaswa kuwashtumu vikali na kuwaonya. Mazungumzo kama haya ndiyo hupelekea kuzalisha unyanyapaa ambao mara nyingi huleta upweke. Nao matabibu na wauguzi wanapaswa kuhimizwa kuwashughulikia wagonjwa wa uraibu kama wagonjwa wengine kwa kuwa uraibu ni tatizo la kiafya tu.
Ni vyema jamii izinduke na kupata mwamko pamojana uhamasisho kuwa, uraibu sio uhalifu. Viilevile jamii inapaswa kuhamasishwa na kuelewa kuwa, Kuchukulia swala nzima la matumizi ya dawa za kulevya kama shughuli ya uhalifu kunaweza kuchangia dhana potofu ya watu wanaotumia dawa za kulevya kuwa hatari zaidi kwa jamii
Hivyo basi, waathiriwa wanapaswa kuonyeshwa upendo, kukubaliwa na kuenziwa na familia zao. Hi ni njia moja wapo ya kuwaweka karibu ili wahisi kama watu wakamilifu na pia kuwapa mazingira salamu ya kujieleza kikamilifu. Hivi inakuwa rahisi kuwapa motisha na matumaini kuwa ipo siku waraibu na wale wote wanaotumia mihadarati kuwa, historia na hali yao itabadilika. Ni vyema familia na mrafiki wawe katika mstari wa mbele kuwashawishi ili wapate matibabi na hata kujiunga na vituo vya urekebishaji.