Skip to main content
Photo credit: pexels

Uzuiaji wa Matumizi ya Dawa za Kulevya na Pombe Huanza na Wazazi

Na Rebecca Barasa

Kuna uwezekano mkubwa, watoto katika shule za daraja la chini hawajaingilia matumizi ya pombe na dawa za kulevya na pia hawana ushawishi mkubwa wa kutumia. Huu ndio wakati mwafaka ambao wazazi wanaweza anzisha mazungumzo kuhusiana na hatari za matumizi ya dawa za kulevya na pombe. Kuzuia matumizi ya pombe na dawa za kulevya huanza na wazazi kujifunza jinsi ya kuzungumza na watoto wao kuhusu mada hii.

Mzazi ana athari kubwa kwa uamuzi wa mtoto wake wa kutotumia pombe na dawa za kulevya. Mzazi anapaswa kusaidia na kumwelekeza mtoto wake kufanya maamuzi mazuri na marafiki wazuri. Mfundishe mtoto wako njia tofauti za kusema "Hapana!” hasa anapopata ushawishi wa kuingilia matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

Wazazi ni nguzo tegemezi ya ushawishi mkubwa ambayo watoto wanayo hasa kwa kuadilisha familia kwa jumla. Hakuna hakikisho kwamba mtoto wako hatatumia dawa za kulevya, lakini matumizi ya vileo na dawa za kulevya hayana uwezekano mkubwa kutokea ikiwa mzazi atasimama imara na kutoa mwongozo na sheria wazi kuhusu kutotumia mihadarati. Sharti mzazi awe kielelezo kwa wanawe kwa kuepuka mihadarati ili nao waige mfano huo huo. Zungumza kwa uaminifu na mtoto wako kuhusu maamuzi mazuri na tabia hatari. Sikiliza mtoto wako ana maoni yepi kuhusu dawa za kulevya ili kupata uelewa wake kuhusu swala hili.
 Vile vile, mweleze mtoto wako kuhusu athari za pombe na dawa za kulevya kwenye akili na mwili wake. Yafanye mazungumzo kuhusu kuepuka pombe na matumizi ya dawa za kulevya kuwaa utamaduni katika familia yako ili wanao wapate kuelewa kwa kina na kuepuka.

Sahihisha imani yoyote potofu ambayo mtoto wako anaweza kuwa nayo kuhusiana na mambo ya dawa za kulevya. Yapo mambo mengi ambayo yanasambazwa ambayo yanaweza kuwa kichecheo cha mwanao kuingilia matumizi ya dawa za kulevya na vileo vingine. Mfano;"Kila mtu anakunywa.""Bangi haitakuumiza."

Epuka programu za televisheni, sinema, na michezo ya video inayosifia pombe, na dawa za kulevya. Kwa kuwa ni vigumu kuepuka ujumbe unaopatikana katika muziki na utangazaji, jadili na mtoto wako ushawishi ambao ujumbe huu unao hasa kwa maisha ya familia yako. Tafuta muda wa kufanya mambo pamoja. Kula pamoja mkiwa familia ni wakati mzuri wa kuzungumza na kujifunza kuhusu kile kinachoendelea.

Mbali na hayo, ni jukumu la mzazi kutumia upendo na uzoefu kurekebisha makosa na chaguo mbaya. Kwa kutumia mchanganyiko wa sifa na ukosoaji, unaweza kurekebisha tabia ya mtoto wako bila kusema mtoto wako ni mbaya. Hii huwasaidia watoto kujenga kujiamini na kumakinika katika kufanya uamuzi wenye busara. Wahakikishie watoto kuwa unawajali ili wajione kuwa wa thamani na kukubalika katika familia. Msaidie Mtoto Wako Kufanya Maamuzi na kujenga urafiki Mzuri.
Ni wazi kuwa, hakuna umri wa chini ulimwenguni ambao unakisiwa kuwa ndio umri wa kuanza kuingilia dawa za kulevya. Hivyo basi, wazazi wanafaa kuwa kwenye mstari wa mbele na kutilia mkazo kutimiza malezi ya viwango vya juu. Kimsingi, hizi ni juhudi ambazo wazazi wanaweza tumia ili kujenga misingi dhabiti ya Maisha ya wanao ya usoni kwa kufanya uzuaji wa mapema.